30 Desemba 2023 - 16:56
Idadi ya waliofariki Gaza katika mashambulizi ya Israel tangu Oktoba 7 imefika 21,500

Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na jeshi katili la Israel huko Gaza tangu Oktoba 7 imeongezeka hadi 21,507, huku 55,915 wakijeruhiwa.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Ijumaa Wizara ya Afya katika eneo hilo lililozingirwa.  Aidha aghalabu ya waliouawa katika vita hivyo vinavyoungwa mkono na Marekani dhidi ya Gaza ni wanawake, watoto na raia wasio na hatia.

Maelfu zaidi pia hawajulikani waliko na inaaminika wamekufa chini ya vifusi. Halikadhalika taarifa zinasema mashambulizi ya Israel yamesababisha Gaza kuwa eneo lililojaa  magofu, huku 60% ya miundombinu ya eneo hilo ikiharibiwa na karibu wakaazi milioni 2 wamelazimika kuyahama makazi yao huku kukiwa uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na madawa.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limeonya kwamba asilimia 40 ya wakazi wa Gaza wako katika hatari ya njaa huku utawala dhalimu wa Israel ukizuia kuingia kwa lori za misaada ya dharura katika eneo hilo.Hayo yanajiri wakati ambao Idara ya Vyombo vya Habari ya serikali ya Ukanda wa Gaza imeutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa unaiba viungo vya miili ya Wapalestina wanaouawa katika mashambulizi ya utawala huo kutoka kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na imetoa wito wa kuundwa kamati huru ya uchunguzi wa kimataifa ya kufuatilia suala hilo.

Naye mratibu wa timu za matibabu ya dharura katika Shirika la Afya Duniani, Sean Casey, ambaye ameshiriki katika operesheni ya kibinadamu katikati mwa Gaza, amesema damu zimetapakaa kila mahali katika hospitali za eneo hilo na kwamba alichokiona huko ni mito ya damu na chinjachija ya binadamu" akisisitiza kwamba hakuna mahali salama katika eneo hilo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijaweza kutekeleza majukumu yake ya kuzuia mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel  huko Gaza kutokana na Marekani kutumia kura yake ya veto kuhusiana na mzozo huo.


342/